Baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salam, wakiwa nje ya Ukumbi wa Nkrumah uliopo kampasi kuu ya chuo hicho.
Ukipata fursa ya kuonana na kuongea na daktari bingwa yeyote wa magonjwa ya watoto au yule wa afya ya kinywa na meno, miongoni mwa ushauri mkubwa atakaokusisitizia ni ule wa kutowapa watoto wako vyakula vyenye sukari kwa wingi hasa biskuti, pipi au keki.
Madhara yatokanayo na kuupuzia ushauri huu huwa ni kuoza kwa meno na hatimaye mtoto huyu kujikuta akiwa kibogoyo katika umri mdogo kabisa wa maisha yake.
Mfumo wa elimu unaotumika kuwaandaa wasomi wetu nchini na barani Afrika kwa ujumla ni wazi kabisa umekuwa ukitengeneza vibogoyo kwa miaka nenda rudi. Kwa faida ya makala haya, kibogoyo ni mtu asiye na meno au kwa lugha rahisi mtu asiye na madhara kwa vitu vitamu kama nyama, mahindi ya kuchoma au karanga.
Nchini Tanzania kijana hupitia mfumo wa elimu wa takribani miaka 16 mpaka kuwa mhitimu wa chuo kikuu. Huanza na miaka saba ya elimu ya msingi, miaka minne ya sekondari na mingine miwili ya sekondari ya juu na baadaye kuanza miaka mingine mitatu hadi mitano ya elimu ya juu.
Kwa matarajio ya kawaida tunategemea msomi wa shahada ya utawala katika biashara aliyetumia zaidi ya muongo mmoja na nusu akiwa shule, atakuwa msaada mkubwa kwa mamalishe pale mtaani asiyezingatia utunzaji bora wa mahesabu na asiye na dira yoyote au maono makubwa ya biashara yake ya chakula
Tunategemea msomi wa shahada ya kilimo na ufugaji atakuwa mkombozi mkubwa wa mkulima pale kijijini kwake kwa kumpa mbinu za kisasa za kilimo na kumuunganisha na wadau muhimu wa kilimo walioko ndani na nje ya nchi.
Wasomi wasio na tija
Tofauti na matarajio hayo, wasomi wetu wamegeuka vibogoyo! Hawana meno, hawang’ati, hawatishi tena, wamegeuka kuwa matanuru ya lawama zisizokwisha dhidi ya Serikali yao, wazazi wao na Taifa lao.
Ukizunguka katika taasisi mbalimbali nchini utakutana na vioja lukuki juu ya wasomi hawa. Mabenki na taasisi nyingi za fedha wafanyakazi wa madirishani (bank tellers) ni wahitimu wa masuala ya sayansi na kompyuta badala ya wataalamu wa fedha.
Wasomi waliobobea katika kilimo au ufugaji wamejivika utaalamu wa fedha na utawala katika biashara! Siasa za nchi kwa maana ya nafasi za ubunge na udiwani, ukuu wa mikoa na wilaya wameachiwa wafanyabiashara, wahandisi na wastaafu wa fani zisizo na taaluma ya siasa, ilhali wataalamu wa sayansi ya siasa wakisukumana kupata ajira ndani ya jeshi.
Nani wa kulaumiwa?
Nani wa kulaumiwa katika hili? Je, ni Serikali inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa zaidi ya nusu karne sasa au wasomi hawa waliogeuka vibogoyo?
No comments:
Post a Comment