Natambua kuwa kwa sababu mbalimbali, walengwa husika wa makala haya hawatosoma mawazo yangu, lakini wewe utakayebahatika kunisoma kwa pamoja, mimi na wewe tuna dhima ya kuwanusuru vijana wa Taifa hili.
Sote ni mashahidi wa hali ya vijana wengi mjini na vijijini, vijana wanasikitisha; hawana mwelekeo na hawajielewi.
Katika Taifa lenye kila aina ya rasilimali, vijana wakiwamo wasomi wanashindwa kuzichangamkia. Wamebaki kuwa walalamikaji. Wengi wanasuburi ajira kama vile zinaletwa katika mfuko.
Kibaya zaidi wale waliotarajiwa kuwapa ajira hizo au pengine kuwajengea mazingira ya kuhimili vishindo vya maisha, wamewatosa. Wanajali matumbo yao na familia zao.
Wamebaki kuwatungia sera na kuanzisha mipango ya kudunisha vipawa na elimu yao, ilhali wao wanasomesha watoto wao nje ya nchi kwenye elimu inayowawezesha kukabiliana na changamoto za dunia ya kileo.
Matokeo ya kususwa kwa vijana wa nchi hii kila mwenye akili timamu anayaona. Vijana wamejaa vijiweni hawajui leo wala kesho yao. Hata wanapobahatika kutia kitu mfukoni wanaishia kupeleka katika michezo ya kamari.
Leo vijana wengi wamekumbwa na pepo la ‘kubet’ (kubashiri michezo ya mpira wa miguu). Mwelekeo na mawazo ya kupambana na maisha vimeelekezwa katika kubashiri mipira na aina nyingine za michezo ya kamari badala ya kazi.
Kuna mwanasiasa mmoja amewahi kusema vijana wasio na ajira ni bomu linaloweza kulipuka muda wowote. Kabla halijalipuka mimi na wewe angalau tufanye kitu; tuwasaidie vijana baada ya kutoswa na wenye haki zaidi ya kufaidi matunda ya nchi hii.
Tufanyeje? Kwa kuanzia vijana hawa hawahitaji mitaji, kwani kwa namna walivyovurugwa, nina wasiwasi kuwa wanaweza kutapanya mitaji hiyo. Tuwape elimu ya kujitambua kwanza, wayajue maisha na wajibu wao katika kupambana na changamoto zake.
Tuwajenge wabadili mtazamo kuwa maisha bora hayapatikani kwa ‘kuyakatia denge’. Waelezwe ukweli kuhusu kanuni za maisha kuwa mafanikio ya kweli hayatokani na njia za mkato. Wajue kuwa dunia ina watu wachache mno waliowahi kutoka kimaisha kwa kupitia mgongo wa kamari.
Badala ya kuwaacha waendelee kulalamika wakiisubiri Tanzania ya asali na maziwa ambayo haipo kwao isipokuwa kwa wateule wachache, tuwaeleze wabadili fikra kuwa maisha yanawezekana tena popote. Tena jambo zuri ni kuwa wenyewe wana msemo wao siku hizi usemao: kambi popote.
Tuwaeleze kuwa hakuna mwanasiasa mwenye dhamira ya kuwatoa kimaisha, zaidi ya kuwatumia kama daraja la kuwawezesha viongozi wa kisiasa kutimiza matakwa yao binafsi.
No comments:
Post a Comment