Pichani ni katibu mkuu wa yanga Jonas Tiboroha
Nyota watatu wa Yanga, Simon Msuva, Mliberia Kpah Sherman na Mbrazil Andrey Coutinho, wanatarajia kuondoka nchini mwezi ujao kuelekea Ureno kwa ajili ya kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa.
Akizungumza na NIPASHE jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Jonas Tiboroha, alisema wachezaji hao wametakiwa kwenda kufanya majaribio katika klabu moja ya daraja la pili na kama watafuzu watasajili baada ya mazungumzo kukamilika.
Alisema mwaliko huo unawataka wachezaji hao kwenda Agosti mwaka huu na kwamba wataitumikia Yanga katika michuano ya Kombe la Kagame na baada ya hapo ndipo watakwea pipa kuelekea Ureno kujaribu bahati yao.
"Lengo letu ni kuwapeleka wachezaji hao kwenye timu nzuri ili waitangaze klabu ya Yanga. Wanatarajia kufanya majaribio kwa muda wa wiki mbili hadi tatu na kama wakifuzu tutafanya mchakatato wa kusajili wachezaji wengine kwa ajili ya kuziba nafasi zao kabla ya ligi kuanza.
"Nitafute baadaye kidogo nitakueleza klabu wanayoenda kufanya majaribio," alisema Tiboroha.
NIPASHE lilipomtafuta baadaye hakupatikana kwa namba yake ya simu ya mkononi, hata hivyo gazeti hili litaendelea kumtafuta kuweza kuwajuza klabu iliyotoa mwaliko wa majaribio kwa nyota hao.
Katika hatua nyingine, katibu huyo alisema Yanga imejipanga kuhakikisha msimu huu inafanya vizuri kwenye Ligi Kuu Bara na Kombe la Kagame kutokana na maandalizi mazuri walioyafanya.
Tiboroha alisema tayari wamefanya maandalizi ya kutosha kuivaa Gor Mahia ya Kenya katika mechi ya ufunguzi ya Kombe la Kagame Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Alisema anaamini mechi tatu za kirafiki Yanga ilizocheza chini ya Kocha Mkuu, Mholanzi Hans van der Pluijm na msaidizi wake, Boniface Mkwasa, zimewasaidia kukiandaa kikosi chao hasa ukizingatia wachezaji walipaswa kuzoeana kutokana na baadhi kusajiliwa katika dirisha hili la usajili linaloendelea.
Michuano ya Kombe la Kagame inatarajiwa kuanza Jumamosi wakati Ligi Kuu Bara ikianza kufurukuta Agosti 22, mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment