.

.

TUMIA VIDOLE

TUMIA VIDOLE
PATA HABARI MBALI MBALI KUTOKA KATIKA BLOG HII PIA TANGAZA AU TOA MAONI KUPITIA Email:Luzunhowhiser@gmail.com OR Cell: 0653394330 OR 0755560918 PATA HABARI MBALI MBALI KUTOKA KATIKA BLOG HII PIA TANGAZA AU TOA MAONI KUPITIA Email:Luzunhowhiser@gmail.com OR Cell: 0653394330 OR 0755560918sundwa.Blogspot.com

Tuesday, July 28, 2015

Ikulu yacharukia uzushi wa gazeti

SERIKALI imekanusha taarifa ya gazeti la Mwananchi, inayosema kuwa Rais Jakaya Kikwete ni miongoni mwa marais watano wa Afrika wanaolipwa mishahara minono barani Afrika.

Imesema kuwa habari hiyo siyo za kweli, imejaa uongo, uzandiki na uzushi tena wa hatari.

Aidha, imesema mshahara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwezi ama kwa mwaka, haufikii na hata wala kukaribia kiwango kinachotajwa na gazeti la Mwananchi cha dola 192,000 (karibu Sh milioni 400) kwa mwaka, sawa na dola 16,000 kwa mwezi, sawa na Sh milioni 33.2. Dola moja kwa sasa ni sawa na Sh 2,077.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari, si Rais Kikwete tu, bali tangu Uhuru mwaka 1961, Rais wa Tanganyika na baadaye tangu mwaka 1964 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amekuwa miongoni mwa viongozi wanaolipwa mishahara ya chini kabisa duniani.

“Mshahara wa Rais wa Tanzania kwa mwezi ni wa chini kiasi cha kwamba mshahara wake unazidiwa, tena kwa mbali, na mishahara wanayolipwa baadhi ya watendaji wakuu wa baadhi ya taasisi za umma nchini,” ilieleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilikuwa inajibu habari, iliyochapishwa katika toleo lake la jana la gazeti hilo katika Ukurasa wake wa 26, iliyosomeka “Marais watano wanaotajwa kuongoza kwa mishahara minono barani Afrika ni hawa hapa”.

Katika habari hiyo ambayo gazeti hilo, linadai chanzo chake ni “Uchambuzi wa Mtandao wa African Review”, inadaiwa kuwa Rais Kikwete anashikilia nafasi ya tano miongoni mwa viongozi 38 wa nchi za Afrika, wanaolipwa mshahara mnono zaidi. “Habari hizi siyo za kweli. Ni uongo na uzandiki. Ni uzushi mtupu na ni uzushi wa hatari. Mshahara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwezi ama kwa mwaka haufikii na hata wala kukaribia kabisa kiwango kinachotajwa na gazeti la Mwananchi,” ilisisitiza taarifa hiyo.

Iliongeza kuwa; “Ni jambo la kushangaza kwamba gazeti la Mwananchi, linalochapishwa hapa nchini, linaweza kupata kiasi cha uongo anacholipwa Rais wa Tanzania katika mitandao ya nje badala ya kuuliza rasmi na kupewa majibu sahihi.”

“Kwa kujiingiza katika uzushi wa kupindua kiasi hiki, gazeti la Mwananchi haliwezi kuwa na nia nyingine yoyote isipokuwa nia ya kuwachochea wananchi na kuwajengea chuki dhidi ya Serikali yao na Kiongozi wao Mkuu. “Ni matarajio yetu, kuwa gazeti la Mwananchi litafanya jitihada za makusudi, kama taaluma ya uandishi wa habari inavyoelekeza, kutafuta usahihi wa jambo hili na kuwaambia Watanzania ukweli.”

No comments:

Post a Comment