ALIYEKUWA Mbunge wa Viti Maalumu, Leticia Nyerere (Chadema) amesema ametua mzigo mzito wa miaka mitano baada ya kutangaza rasmi kurudi Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Aidha, amesema suala la kuhamia Chadema hakutafakari kwa kina na kwamba kama angetafakari, asingeweza kwenda huko.
Huyo anakuwa mbunge wa pili wa Chadema kurejea CCM, mwingine ni Philipa Mturano ambaye siku chache baada ya kuachana na Chadema, ameshinda kura za maoni katika mchujo wa wagombe wa Viti Maalumu ndani ya CCM, akipitia mkoani Kigoma.
Leticia alisema hayo jijini Dar es Salaam jana alipokuwa anazungumzia kuachana na Chadema alichokitumikia kwa miaka mitano.
Alisema baada ya kujiengua Chadema, mchango wake unatambulika na kwamba sasa anaweza kutumikia CCM nje bila ya kuwa mbunge na kuweza kuleta maendeleo kutokana na uwezo wake katika masuala ya siasa.
“Moyo wangu umekuwa ukisononeka kutokana na kukaa Chadema na kuacha kukaa katika chama kilichonilea na kunisomesha hadi nje ya nchi ,sasa nasema narudi nyumbani kutumikia,” alisema na kuongeza kuwa, alipokelewa vyema na kupewa ushirikiano Chadema, lakini siku zote nafsi yake imekuwa ikimsuta,” anasema.
Anaongeza kusema: “Kwa kipindi chote nilikuwa nikiumia sana na kila sehemu bora, isipokuwa nyumbani ni bora zaidi, hivyo nimeamua kurudi kwenye chama ambacho kimenilea na kunipa elimu na watoto”. “Yawezekana nilikurupuka nikaenda ugenini, ingawa walinipokea vizuri lakini ukiwa wa kusema sipo nyumbani ulinitesa sana na wakati mwingine waliniona wa kuja,” alisema.
Alipoulizwa ni kitu gani amekutana nacho Chadema hadi kuamua kurudi CCM, hakufafanua zaidi na kusisitiza kwamba dhamira yake ni kubwa yenya ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya katika kukijenga chama chake cha Mapinduzi.
“Leo nimetua mzigo mzito nilioubeba kwa miaka mitano na hakuna aliyepo upinzani ambaye siyo mhamiaji wote walikuwa CCM na hii nilichokuwa nimekifanya ni upuuzi usiokuwa na thamani,” alisema. Hata hivyo, alipoulizwa hatma yake kisiasa, alisema amedhamiria kukijenga chama kwa nguvu zake zote bila kujali nafasi atakayokuwa nayo.
No comments:
Post a Comment