Baadhi ya wananchi mkoani hapa wamememtaka mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli (Pichani), kuepuka visasi na kusikiliza makundi yote ya kijamii endapo atachaguliwa kuwa Rias wa Tanzania uchaguzi mkuu ujao.
Wakizungumza na NIPASHE mjini hapa kuhusu uteuzi wa Dk. Magufuli, baadhi ya wananchi wakiwamo makada wa vyama mbalimbali vya siasa, watumishi wa umma na wakulima, walisema wanaimani na uteuzi huo na kumtaka Magufuli kuwa kiongozi wa Watanzania wote bila ya kufanya ubaguzi.
Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika wa Wakulima wa Matunda na Mbogamboga cha Busanda, Elias Kisome, alisema wana matumaini makubwa na Dk. Magufuli.
Kwa upande wake, Mwalimu wa Shule ya Sekondari, Salehe Kabaju, alisema kuchaguliwa kwa Dk. Magufuli kuwa mgombea urais wa CCM kumerejesha matumaini mapya kwa Watanzania wakiwamo watumishi wa umma kwani wana imani ataboresha maisha yao na uwajibikaji wake utasaidia kila mtu kujituma katika eneo lake la kazi kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
Naye Mchungaji wa Kanisa la Methodist Huru Tanzania (FMCT) Jimbo la Geita Wilayani Chato, Cosmas Bitoye, anakotoka mgombea huyo wa CCM, alimuelezea Dk. Magufuli kuwa ni mtu jasiri na mchapakazi na kumtaka wakati wa uongozi wake kuongozwa na hofu ya Mungu.
Askofu Musa Magwesera wa Jimbo la Geita Kansia la African Inland Tanzania (AIC), alisema anamfamu vizuri Dk. Magufuli, lakini hawezi kutoa maoni yake hadi hapo vyama vingine navyo vitakapotangaza wagombea wao ili kuona mwenye sifa ya kufaa kuongoza nchi.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment