Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungi.
Wadau wa mawasiliano mkoani hapa, wameiomba Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kudhibiti matumizi mabaya ya simu za mkononi na mitandao hususani katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika nchini Oktoba 25, mwaka huu.
Wadau hao walitoa rai hiyo juzi mjini hapa, kwenye warsha iliyotolewa na TCRA kwa lengo la kuwakumbusha wananchi manufaa ya mawasiliano.
Wadau hao walisema kadri siku za uchaguzi zinavyokaribia, ndivyo ujumbe wa kupigana vijembe kwa lengo la kuchafuana kisiasa zinazidi kukithiri na kuendelea kuwachanganya wananchi.
Akizungumza kwenye warsha hiyo, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Njombe, Edward Mgaya, aliwataka wananchi wasitumie simu zao vibaya kwa kuchafuana au kufanya malumbano kwenye mitandao ya kijamii hasa wakati huu wa uchaguzi.
“Ndugu zangu wananchi wa Njombe ninawaombeni kipindi hiki cha uchaguzi tumieni simu zenu vizuri msichafuane ili muweze kufanya uchaguzi kwa amani na mpate kiongozi atakayewatatulia changamoto zenu, ”alisema.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi waliohuduria warsha hiyo, walitoa tahadhari ya matumizi ya simu kifamilia kwa kutopokea picha zinazoweza kuhatarisha au kuvunja ndoa zao.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Pindi Chana, aliwataka wakazi wa Njombe kutumia mawasiliano ya simu kutafuta masoko ya mazao yao.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk. Rehema Nchimbi, aliitaka Mamlaka hiyo kupunguza gharama za simu.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungi (pichani), amewaondoa hofu wananchi wanaoishi karibu na minara ya mawasiliano kuwa haina madhara kwao.
Mungi alisema hakuna mionzi yoyote inayoweza kuwadhuru wananchi kwa sababu minara hiyo imefungwa vifaa muhimu na vyenye kiwango vya kimataifa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment