Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP ), Ernest Mangu.
Wakati bado hakuna mtuhumiwa aliyekamatwa kufuatia tukio la kuvamiwa kwa Kituo cha Polisi cha Stakishari, jijini Dar es Salaam, imefahamika kuwa bunduki zilizoibwa ni 20, huku Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP ), Ernest Mangu (pichani), akitangaza bingo ya Sh. milioni 50 kwa mtu atayekatoa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwa majambazi waliofanya tukio hilo.
Watu wanaosadikiwa kuwa majambazi walikivamia kituo hicho usiku wa kuamkia Julai 12, mwaka huu na kuwaua askari polisi wanne, raia watatu na kisha kupora silaha kadhaa na kutokomea nazo kusikojulikana.
Kwa nyakati tofauti, IGP Mangu na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, kila wanapoulizwa idadi ya silaha zilizoporwa na majambazi hayo, wamekuwa wakishikwa kigugumizi kusema.
Hata hivyo, taarifa zilizothibitishwa na baadhi ya askari wa kituo cha Stakishari zimeeleza kuwa jumla ya silaha zilizoporwa katika kituo hicho ni 20 ambazo ni aina ya Sub Machine Gun (SMG).
“Kimsingi majambazi waliovamia kituo chetu siyo majambazi wa kawaida hawa ni magaidi, wamepora SMG 20…Hali inatisha, “alisema askari polisi mmoja wa kituo hicho wakati akizungumza na NIPASHE.
Wakati hayo yakiendelea, Mkuu wa jeshi hilo, Mangu ametangaza zawadi ya Sh. milioni 50 kwa mtu yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwa majambazi waliovamia kituo hicho.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Kova, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa tukio hilo wamelichukulia kwa uzito wa kipekee na wanafanya jitihada za kufa na kupona kuhakikisha wahalifu waliohusika wanakamatwa.
Kamishna Kova alisema katika kukabiliana na majambazi wanaovamia vituo vya polisi, zitafungwa kamera za CCTV katika vituo vyote vya polisi nchini.
Aliongeza: “IGP ameamua kutoa fedha hizo ili kumzawadia atakayefanikisha kupata taarifa za wahalifu, fedha hizo zipo tayari na tunawahakikishia kwamba tutamlinda mtoa taarifa na zawadi yake tutamkabidhi kimya kimya kama ambavyo tumekuwa tukifanya vipindi vilivyopita.”
Alisema hadi sasa bado hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo na kwamba Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kuhakikisha wahalifu wanatiwa mbaroni.
Kova alitaja baadhi ya namba za Makamanda wa Polisi watakaokuwa wanapokea taarifa za watoa taarifa za watuhumiwa kuwa ni 0754 034224 ya kwake mwenyewe, Msemaji wa Jeshi hilo, Advera Bulimba (0713 631667) na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athumani 0715 323444.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment