Mechi hiyo ya ufunguzi itatanguliwa na mchezo mwingine wa utangulizi utakaozikutanisha APR ya Rwanda dhidi ya Al Ahly Shandy ya Sudan utakaofanyika kuanzia saa nane mchana huku nyingine kati ya KMKM ya Zanzibar itakayowakaribisha Telecom ya Djibout ikichezwa saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Karume, Ilala jijini.
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto, alisema jana kuwa maandalizi ya mashindano hayo yako katika hatua za mwisho na klabu wenyeji zimejipanga kupeperusha vyema bendera ya nchi.
Kizuguto alisema timu zinazoshiriki mashindano hayo zinatarajiwa kuanza kuwasili nchini kuanzia leo na kwamba APR itatua saa tisa mchana ikifuatiwa na Gor Mahia itakayokuja kesho.
Alisema mchezo huo wa ufunguzi kati ya Yanga dhidi ya Gor Mahia unatarajiwa kuwa na ushindani na kuteka 'hisia' za mashabiki wa soka wa Ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na klabu hizo mbili kutokutana kwa kipindi cha miaka 19 sasa.
Aliongeza kuwa, mara ya mwisho Yanga inayonolewa na Mholanzi Hans van der Pluijm na Gor Mahia iliyoko chini ya Frank Nuttal, ambaye ni raia wa Uskochi, zilikutana mwaka 1996 katika michuano hii ya Kombe la Kagame hatua ya makundi na kutoka sare ya bao 1-1, wakati zilipokutana katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu, Gor Mahia iliibuka na ushindi wa mabao 4 -0.
Mara ya mwisho Yanga iliyochukua ubingwa huo mara tano, ilishinda kikombe hicho mara mbili mfululizo mwaka 2011 na 2012 mashindano hayo yalipoandaliwa nchini, na mwaka huu inasaka historia ya Simba ambayo imeshinda mara sita.
Katika mashindano ya mwaka huu, Yanga inatarajia kuwatumia wachezaji wake wapya iliyowasajili ambao ni pamoja na Donald Ngoma, mshambuliaji aliyesajiliwa kutoka Platinum ya Zimbabwe, Joseph Zutta wa Ghana, Malimi Busungu (Mgambo JKT) na Deus Kaseke.
Rekodi kwenye Kombe la Klabu Bingwa:
Yanga imebahatika kutwaa ubingwa mara tano: (Mwaka 1975, 1993, 1999, 2011, na 2012).
Pia Yanga imemaliza kama mshindi wa pili mara mbili, mwaka 1976 ilipofungwa na Gor Mahia 2-1 jijini Kampala na 1992 ilipolala kwa mikwaju ya penalti mbele ya watani wao wa jadi, Simba.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment