
HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam imeiomba serikali kuu kulisuka upya jiji hilo kimuundo ili liwe na nguvu kisheria ya kutekeleza majukumu yake, kwa kuwa hivi sasa linashindwa kutokana na kuingilia mamlaka nyingine, hivyo linaonekana halifanyi kazi.
Hayo yalibainishwa jana jijini hapo na Meya wa Jiji hilo, Dk Didas Masaburi kwenye kikao maalumu cha Baraza la Madiwani wa Jiji la Dar es Salaam, lililokutana kwa ajili ya kuvunjwa rasmi kwa baraza hilo, kama ambavyo sheria ya kuundwa kwake inavyoelekeza.
Katika kikao hicho kilichowakutanisha wajumbe wa baraza hilo, Meya wa jiji hilo alisema moja ya changamoto zinazolikabili jiji la Dar es Salaam ni muundo wake ambao kisheria unaingiliana na mamlaka nyingine kiutendaji, hivyo kukosa nguvu ya kutekeleza majukumu yake.
“Ni kweli jiji letu lina tatizo la kimuundo, ambalo linasababisha jiji kukosa nguvu za kisheria kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake na hivyo linaonekana halifanyi kazi, ni vyema serikali ikaona sasa haja ya kuliduka upya kimuundo”, alisema Dk Masaburi.
Awali wakati wa kikao hicho, Mkurugenzi wa Jiji hilo, Wilson Kabwe alielezea mafanikio ya jiji hilo kwa kipindi cha miaka mitano ya uwepo wa baraza hilo ni pamoja na ujenzi wa vituo vya kisasa vya mabasi ya mikoani cha Mbezi Louis na Boko Basihaya pamoja na ujenzi wa miundombinu ya barabara.
Aidha alisema miradi kadhaa iko kwenye hatua za utekelezaji kama mradi wa uendelezaji makazi kwenye viwanja vitatu tofauti katika maeneo ya Kinondoni na Oysterbay jijini hapo.
Pamoja na mafanikio hayo, Kabwe alisema zipo changamoto kama ambavyo Meya ya jiji hilo alivyoeleza na kuongeza kuwa katika utekelezaji wa majukumu yao, hujikuta wakishindwa kwa kuwa maeneo ya utekelezaji yako kwenye mamlaka nyingine kama vile Manispaa, na wakati mwingine huitaji kibali kutoka kwenye Manispaa husika.
“Kwa kweli kuna ugumu wa kutekeleza majukumu ya kazi zetu, jiji lina tatizo la kimuundo, na unapotekeleza kazi zako unakuta unashindwa kwa kuwa unaingilia mamlaka nyingine ambazo nazo ziko kisheria,” alisema Kabwe.
Awali kabla ya kuvunjwa kwa baraza hilo, madiwani walihoji ulipwaji wa posho zao jambo, ambalo Mkurugenzi alilitolea ufafanuzi na kusema wataendelea kupewa posho zao za kila mwezi hadi ifikapo Oktoba kama sheria inavyosema, na kwamba mafao yao yatatolewa na serikali kuu mwisho wa ukomo, ambao ni Oktoba mwaka huu.
Baraza la Madiwani wa Jiji la Dar es Salaam liliundwa Januari 7, mwaka 2011.
No comments:
Post a Comment