KIPINDI hiki cha mchakato wa uchaguzi mkuu, tunawashuhudia Watanzania halisi. Tunaona jinsi majungu na umbea unavyopikwa kuhusu uchaguzi.
Huyu anasema hivi tena kwa uhakika kabisa na yule anasema vile tena kwa uhakika. Mwishowe unagundua wote ni waongo.
Ni kipindi ambacho tutasikia mengi, kuna ambao watakwambia kigogo huyu anakwenda Ukawa, wengine watasema kigogo yule anakwenda CCM. Kinachofurahisha kila mtu anazungumza kwa uhakika kabisa huku akiapa kwa miungu yote.
Siasa zimekuwa kama soka la Bongo, ambapo utasikia Kelvini Yondani wa Yanga kasaini Simba, mwingine atakwambia Emmanuel Okwi kasajiliwa Yanga baada ya kushindwana na klabu yake mpya ya Sonderjskye Fodbold ya Denmark.
Tena kila mmoja atakwambia habari hizo kwa uhakika, atakuapia mpaka atalamba mchanga, lakini siku ya pili utagundua kuwa alikuingiza chaka. Kwa kifupi Watanzania tumezoea kuingizana chaka.
Nani anakumbuka habari ya Simon Msuva na Mrisho Ngassa, ambao msimu uliopita walicheza Yanga kwa mafanikio makubwa hata kuipa ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Bado tunakumbuka kuwa Msuva alikataliwa na Yanga kwenda kufanya majaribio katika klabu ya Bidvest ya Afrika Kusini, mpaka baadaye yeye mwenyewe akatoroka kwenda bondeni, lakini kwa bahati mbaya alishindwa majaribio.
Bado tunakumbuka jinsi Yanga ilivyomkatalia Ngassa kwenda kufanya majaribio katika klabu ya Free State ya Afrika Kusini, lakini mwenyewe alitoroka na kwenda kufanya majaribio katika nchi hiyo ya Madiba na bahati nzuri alifuzu.
Kwa hiyo ndani ya miezi michache iliyopita tumeshuhudia Yanga ikiwakatalia wachezaji wake wawili kwenda kufanya majaribio katika klabu za nje.
Kwa upande wa pili, tumeshuhudia Simba ikiwaruhusu wachezaji wake wawili kufanya majaribio katika klabu mbili za nje.
Jonas Mkude alipewa ruhusa na Simba kwenda Bidvest ya Afrika Kusini, lakini kwa sababu ameshindwa majaribio amerejea katika klabu yake ya Msimbazi jijini Dar es Salaam.
Simba pia ikampa ruhusa Emmanuel Okwi kwenda katika klabu ya Ligi Kuu Denmark inayoitwa Sonderjskye Fodbold ambako amepata mkataba wa miaka mitano.
No comments:
Post a Comment