WATANZANIA 4,200 kutoka mikoa mitano nchini wamenufaika na mpango wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) wa kupeleka madaktari bingwa mikoani.
Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti wa NHIF, Raphael Mwamoto alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mpango huo.
Alisema wananchi hao walionwa na madaktari bingwa na kati yao takribani 100 walifanyiwa upasuaji kulingana na magonjwa walikuwa nayo.
“Tumeubuni mpango huu kwa ajili ya kusaidia wananchi wa pembezoni. Madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili na MOI pamoja na wa hospitali ya rufaa katika eneo husika huweka kambi kwa ajili ya kuwahudumia wananchi,”alisema.
Katika awamu ya kwanza ambayo imehusisha mikoa ya Lindi, Kigoma, Katavi, Rukwa na Pwani, mfuko umetumia takriban sh milioni 180.
Alisema awamu ya pili ya mpango huo ifanyika kati ya Novemba 3 hadi 8 mwaka huu mkoani Mara na kambi itakuwa katika hospitali ya Rufaa, hivyo kuwahamamisha wananchi kujitokeza kwa wingi muda utakapowadia.
Madaktari hao bingwa ni wa magonjwa ya moyo, kinamama, watoto, upasuaji na mabingwa wa dawa za usinguizi.
Pamoja na hilo, amewahamaisha wananchi kujiunga na mfuko huo, ili wawe na uhakika wa matibabu.
Wakati huohuo, mfuko huo umesema umelipa sh bilioni 110 kwa mwaka wa fedha 2013/2014 kwa hospitali
zinazohudumia wanachama wake kwa ajili ya ununuzi wa dawa na huduma nyinginezo.

No comments:
Post a Comment