MWENYEKITI wa Baraza la Wanawake CHADEMA, (BAWACHA), Halima Mdee, amesema kuwa katika kipindi cha miaka tisa ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete, deni la Taifa limeongozeka kutoka sh trilioni saba hadi trilioni 30.
Aidha, kila mtanzania bila kujali umri wake, anatakiwa kulipa kiasi cha sh. 680,000 kwa fedha ambazo hakushirikishwa wakati wa kuzikopa.
Mdee, aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na umati mkubwa wa wananchi kwenye viwanja vya Sabasaba mjini Bunda, akiwa ameongozana na Makamu Mwenyekiti, Hawa Mwaifunga, Katibu, Grace Tendega, Naibu Katibu, Kunti Yusuph na Katibu Uenezi BAVICHA, Edward Simbeye.
Mdee ambaye pia ni Mbunge wa Kawe, alisema kuwa Serikali inadai deni hilo limeongezeka kwa sababu ya kupeleka maendeleo kwa wananchi, jambo alilodai kuwa si kweli, kwani katika kipindi hicho hali ya maisha ya wananchi imezidi kuwa duni.
“Jaji Warioba aliliona hili baada ya kusilikiza maoni ya wananchi akaandika kwenye rasimu ya pili suala la uwazi, uadilifu na uwajibikaji liingie kwenye katiba ili kuzuia viongozi wa umma wasiende kukopa fedha nje ya nchi na badala yake wazilete kwa wananchi, wakaingiza kwenye matumbo yao halafu watake wananchi mzilipe….
“Tume ya rais ya mabadiliko ya katiba ilisema kuwa tunataka Rais asipande ndege ovyo kwenda huko majuu kukopa, kwani badala ya kulisaidia taifa wanazidi kuwabebesha mzigo wananchi, hivyo akataka taifa lisikope mpaka bunge liidhinishe baada ya kujulikana tunakopa kwa sababu gani, lakini wabunge wa CCM wameona huu ni upuuzi wametupilia mbali pendekezo hilo la msingi kabisa,” alisema Mdee.
Aliwataka wanawake wasitishwe na propaganda za CCM kwamba, vyama vya vya upinzani vitasababisha vurugu, jambo alilosema kuwa sio kweli kwani CCM ina hofu ya kung’olewa madarakani.
Naye Mwenyekiti wa CHADEMA mkoani Mwanza, Mhandisi Adrian Tizeba, aliwataka wananchi kuiogopa CCM kama ugonjwa hatari wa Ebola.
Alisema CCM imeshindwa kuwapa wananchi maisha bora huku ikiwanyima huduma muhimu, hali inayosababisha wengi wapoteze maisha kwa kukosa huduma za matibabu kwa magonjwa yanayotibika.
Aliwataka wananchi hao waing’oe CCM kwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu mwakani.
Heche aibua ufisadi halmashauri Magu
Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Vijana Taifa, (BAWACHA), John Heche, aliwaeleza wananchi hao kuwa ni ajabu kwa mji wa Magu kutokuwa na maji safi na salama ya bomba wakati uko kilometa sita tu kutoka Ziwa Victoria.
“Maji hapa Magu yanaonekana kuwa anasa kwa sababu hayapatikani, mnatumia maji ya visima na yana chumvi, nyie mnaikumbatia CCM wakati haiwajali…
“Wameshindwa kuwavutia maji pale Ziwa Victoria na ni kilometa sita tu lakini wameweza kuyapeleka mkoani Shinyanga. Hii Serikali ni ya ajabu sana, haiwajali kabisa lakini sasa kwa kuwa uchaguzi unakaribia wataanza kuwaletea kanga na sukari nusu kilo, muwakatae,” alisema Heche.
Alisema kuwa inasikitisha kuona Wilaya hiyo ikikosa zahanati na kituo cha afya ambazo hutoa huduma kwa bei nafuu, hali inayowalazimu kwenda kupatiwa huduma kwenye hospitali ya Wilaya, ambako kumuona daktari pekee ni sh 5,000.
“Kwenye bajeti ya mwaka uliopita Wilaya ya Magu ilitengewa fedha za maendeleo sh bilioni 1.5, lakini wawakilishi wenu hapa wote ni CCM wameshindwa kuzisimamia ziweze kujenga hata zahanati,” alisema.

No comments:
Post a Comment