Shirikisho la kandanda Tanzania (TFF) limemruhusu mlinda mlango Juma Kaseja kujiunga na timu yoyote ikiwa dirisha la usajili linafungwa hii leo, na itakumbukwa kwamba Chama Cha wacheza Soka Tanzania (SPUTANZA) kilipeleka maombi TFF kikitaka imruhusu mchezaji huyo kuwa huru na kujiunga na klabu yoyote hatimaye hilo limefanikiwa.
CHANZO:Shafii Dauda
Katibu mkuu wa TFF Selestine Mwesigwa amethibitisha TFF kumruhusu Kaseja kujiunga na klabu yoyote ambayo atafikianayo makubaliano na atacheza kwa muda wote ambao suala lake la mgogoro na Yanga likiwa linashughulikiwa.
“Wamelete barua kwa maana ya mchezaji Juma Kaseja ameleta barua akiomba kuwa huru kusajili kwenye klabu anayoitaka kwa sasa kwasababu tangu alipoingia kwenye mgogoro na Yanga amekuwa ‘akichoma mahindi’ sasa sisi tumemruhusu Juma Kaseja kwasababu bado anasubiri hatma yake ya mgogoro wa kikazi na klabu yake ya Yanga”.
“Hatujamuondoa kwenye mgogoro na Yanga ila tumemruhusu acheze wakati mgogoro unashughulikiwa na yeye ama wawakilishi wake”.
Kwa upande wake Kaseja, yeye amesema amepokea kwa furaha uamuzi huo uliotolewa na TFF na kukishukuru Chama Cha Wacheza Soka Tanzania (SPUTANZA) kwa kulipigania suala lake lakini mwisho akavikaribisha vilabu vyote vinavyohitaji huduma yake kwa ajili ya mazungumzo na endapo watafikia makubaliano yeye yuko tayari kucheza timu yoyote inayoshiriki ligi kuu Tanzania bara.
“Mimi nimepokea kwa furaha kwasababu kwa muda mrefu sijacheza kwahiyo nilikuwa nahitaji kucheza, nimeruhusiwa nimepokea kwa furaha na nakaribisha timu yoyote ambayo itahitaji huduma yangu basi nitacheza sichagui timu, timu yoyote ambayo inanihitaji kama tutakubaliana mimi nitacheza tu.
Nataka nicheze ligi kuu kwasababu ni ligi ambayo itakuwa na ushindani kwahiyo nataka nicheze ligi yenye ushindani. Nawashukuru SPUTANZA kwa kulipigania suala langu na TFF kwa kuniruhusu nicheze.
CHANZO:Shafii Dauda
No comments:
Post a Comment