Pichani niWanafunzi kama hawa wanasoma katika mazingira magumu. Wanafunzi wa shule ya Kilolo wamekuwa wakikabiliana na changamoto kama hizi na kufanya vizuri katika mitihani yao.
Wakati Shule ya Msingi Vitono iliyopo katika kata ya Uhambingeto wilayani Kilolo, ni moja ya shule Kongwe nchini inayokabiliwa na changamoto mbalimbali za miundo mbinu,lakini yaendelea kufaulisha wanafunzi mwaka hadi mwaka.
Mwaka jana kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Germanus Nyika anasema, waliohitimu elimu ya msingi shuleni hapo mwaka jana ni wanafunzi 61 na 52 wamefaulu kuingia kidato cha kwanza sawa na asilimia 85 ya mpango wa BRN.
Shule hiyo ilianzishwa mwaka 1974 lakini hadi sasa miundombinu yake chakavu haijakarabatiwa.
Ni moja ya shule maarufu wilayani humo, kwa uzalishaji wa wanafunzi wengi wanaoendelea na masomo ya kidato cha kwanza kwa miaka mingi iliyopita, licha ya kwamba wanafunzi na walimu wapo katika mazingira magumu yenye changamoto mbalimbali.
Miongoni mwa changamoto hizo ni uchakavu wa majengo, hivyo kuiomba serikali kuwasaidia yajengwe majengo mapya kwa kusaidiana na nguvu kazi za wazazi na walezi wa shule hiyo.
Mwalimu mkuu Nyika, alisema shule yake inakabiliwa na upungufu wa vyumba vya madarasa, hivyo kuiomba serikali iwasaidie kuwajengea angalau vyumba vichache vya madarasa.
Nyika anasema kuwa, tatizo la ofisi na nyumba za walimu nalo ni kero kwa sababu wanatumia vyumba vya zamani ikiwamo ofisi ambayo imechoka kwa sababu imejengwa tangu shule ilipoanzishwa.
“Walimu wangu wanalazimika kuishi nje ya shule. Siwezi kuwajengea nyumba walimu wanaokuja kufundisha hapa, hivyo inawalazimu kwenda kupanga nje. Shule yangu ina nyumba mbili za walimu ambazo zimechakaa, moja anaishi mwalimu mkuu sina jinsi ya kufanya zaidi ya kuomba serikali itujengee nyumba za walimu ili kuwafanya walimu waweze kuishi hapa,” anasema Nyika .
Kama hiyo haitoshi, ukosefu wa jengo la kufundishia wanafunzi wa elimu ya awali nayo ni changamoto nyingine ,inawalazimu kwenda kuomba majengo ya misheni kwa ajili ya kufundishia wanafunzi wa awali.
Mwalimu Nyika anasema kuwa, licha ya uchakavu wa majengo hayo, pia kuna upungufu mkubwa wa samani mbalimbali, akiwaomba wadau mbalimbali na wanafunzi waliosoma shuleni hapo wanaoishi katika mikoa mbalimbali wakumbuke kuchangia chochote kwa sababu shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ili angalau kuzipatia ufumbuizi zile zilizo ndani ya uwezo wao.
“Shule hii ni kongwe sana, kuna wanafunzi wamepita hapa ambao sasa wana dhamana mbalimbali katika kazi na maisha yao, wadau mbalimbali wanaoguswa kuchangia maendeleo ya shule hii, wakiwamo wanafunzi waliohitimu ambao wanajiajiri kwenye sekta mbalimbali nchini waje angalau waweke mchango wao kwa sababu ni muhimu kusaidia ujenzi wa jamii hii na taifa kwa ujumla,” anasema mwalimu Nyika.
“Elimu haina mwisho… watoto hawa ni hazina ya baadaye, tusipowafundisha kwa makini , Tanzania itakuwa na wataalam ambao wanapikwa kwa ushirikiano wetu, wazazi na serikali ili kuzalisha wataalamu?,” anahoji na kuongeza.
Kama wanavyosema, elimu haina mwisho madarasa haya ndiyo waliyosoma baba na mama zetu, hivyo ni jukumu letu sote kuhakikisha kuwa, wanafunzi hawa wanapata haki yao ya kimsingi kupata elimu hapa.
Mwalimu Nyika alisema kuwa, katika kuhakikisha kuwa wanafunzi wanakua kisaikolojia, kimwili na kiakili.
“ Kushiriki michezo ni haki yao ya kimsingi, lakini hawawezi kushiriki michezo kama hawana jezi za michezo, hapa shuleni tuna changamoto ya vifaa vya michezo ikiwamo mipira, jezi na vinginevyo muhimu,” anasema Mwalimu Nyika
Anaiomba serikali iisaidie shule hiyo kuezeka vyumba vya madarasa mawili, ujenzi wa nyumba za walimu, ofisi ya walimu na kuwapatia samani mbalimbali zikiwamo viti, madawati, meza na vifaa vingine ili kuifanya shule kuwa na mazingira mazuri ya utoaji wa elimu.
Kama hiyo haitoshi, pia aliiomba serikali kuwaongezea walimu angalau wawili wa awali watakaosaidia kuwafundisha watoto hao kabla hawajajiunga darasa la kwanza.
Kwa miaka mingi, shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri mitihani yake ya ndani na ya kitaifa, katika mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi shule imekuwa inafaulisha kwa asilimia kubwa mathalani mwaka jana, wamefaulisha kwa asilimia 85 na kufikia lengo la BRN, ingawa kuna baadhi ya wazazi ambao hawawapeleki watoto wao sekondari na wengine wanawapeleka, lakini hawamalizi masomo kutokana na sababu mbalimbali.
Pia mwalimu huyo anasema kuwa, mtoto anatakiwa kupata haki zake za msingi bila ya kubaguliwa kama ni wa kiume ama wa kike, wote ni watoto wanaostahili kupata elimu bora, chakula na malazi, kupewa muda wa kupumzika, kushirikishwa katika maamuzi ya kifamilia, kusikilizwa, kuheshimiwa na kupewa fursa ya kushiriki katika michezo.
Kuhusu suala la maji shuleni hapo, mwalimu Nyika alisema kuwa, miaka ya nyuma walikuwa na changamoto kubwa ya maji, lakini sasa tatizo hilo limepatiwa ufumbuzi wa maji ya bomba ambayo ikifika kipindi cha mwezi wa 10 na 11 maji yanakuwa kizungumkuti.
Wana matenki manne ya kukingia maji ya mvua wanayoyatumia kwa sasa.
Kuhusu hitaji la walimu shuleni hapo, alisema kuwa kwa sasa wana walimu 13 mmoja yupo masomoni.Shule hiyo ina wanafunzi 462 hivyo wanahitaji serikali iwaongezee walimu 14 ili kujenga mazingira mazuri ya kuhakikisha kuwa utoaji na upatikanaji wa elimu unafanikiwa.
Hata hivyo, kutokana na ufaulu huo,Mwalimu anasema baadhi ya watoto wanashindwa kuendelea na masomo ya sekondari hasa kutoka katika kitongoji cha Dunguya wanaacha shule kwa sababu mbalimbali.
“ Wanafunzi waliofaulu mwaka jana wote wameenda sekondari kwa sababu ya mimi na mwenyekiti wa kitongoji tumewafuatilia kwa ukaribu, hivyo sijasikia tena kama wameshindwa kwenda kwa maana tuliwafuatilia kweli kweli,”anasema Mwalimu Nyika
Kuhusu chakula cha wanafunzi shuleni hapo, Mwalimu huyo amesema kuwa wanafunzi hawali chakula shuleni hapo kwa sababu baadhi ya wazazi hawakuwa waelewa kuchangia chakula kama walivyokubaliana hivyo kulazimika watoto hao kwenda kula majumbani kwao na kuwafanya wanafunzi washinde na njaa na kuathiri usikivu na ufuatiliaji wa masomo.
Amesema kuwa, wanafunzi hao baadhi ya madarasa huingia asubuhi hadi jioni, isipokuwa darasa la tano na la tatu ,hao wanaoingia kwa kupokezana asubuhi na jioni kwa sababu ya ukosefu wa vyumba vya madarasa.
Shule hiyo ilianzishwa mwaka 1974 hadi sasa haijawahi kufanyiwa marekebisho au kukarabatiwa kwa kiwango chochote kile hivyo kuwa katika mazingira ambayo siyo rafiki sana kwa wanafunzi kusomea na walimu kufundishia.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment